Mbio
za kusaka urais kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimezidi
kushika kasi baada ya mtoto wa tano wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu
Nyerere, Charles Makongoro Nyerere kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wakati
Makongoro akichukua uamuzi huo kwa mara ya kwanza katika historia ya
familia ya Mwalimu Nyerere, mkoani Mbeya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais
Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye ameingia kwenye mbio hizo.
Makongoro
Akitangaza
nia yake katika eneo la Mwitongo kijijini Butiama jana, Makongoro
aliwashambulia makada wenzake ndani ya CCM ambao wanaongoza makundi ya
kuwania urais kwa kuwaita ni ‘vibaka’ wanaokivuruga chama hicho kwa
maslahi yao binafsi.
Akitoa
mfano kwa baadhi ya makada wanaoongoza makundi ndani ya chama hicho,
Makongoro aliwataja kwa majina kuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha,Mwigulu
Nchemba na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira.
Alisema
makada hao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia fedha nyingi kuendesha
makundi ya urais na akahoji sababu za kutafuta cheo hicho cha juu kwa
fedha.
"CCM irudishwe kwa wazalendo kwa sababu vibaka wamekuwa na mlengo mbaya wa kukiendeleza chama hicho," alisema.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuwa maradhi ya rushwa ambayo yameiambukiza nchi nzima.
Makongoro
alisema yeye ni mzalendo wa kweli na anataka kuirudisha nchi katika
misingi ya uadilifu endapo CCM itampa ridhaa ya kupeperusha bendera
katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuibuka genge la watu wachache ambao utajiri wao ni wa shaka na umejijenga kwa fedha chafu.
“Ndani
ya chama tawala wamekuwapo ‘vibaka’ wachache… unajua kibaka ni kibaka
tu hata kama kapewa gari la Serikali lina bendera ya taifa mbele atabaki
kuwa kibaka tu.
“Wananijua
vizuri huwa siwaonei haya kuwaambia ukweli, hawa ndiyo wanaotuvurugia
chama na hawamheshimu Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete,” alisema Makongoro.
Katika hotuba yake ambayo alitumia saa mbili, Makongoro alijikita kuzungumzia madhara yanayotokana na rushwa ndani ya CCM.
Alisema
baadhi ya makada wanaotumia rushwa wamezalisha makundi na mipasuko
isiyo ya lazima huku akisisitiza kuwa anachukia kuwapo makundi ndani ya
chama hicho.
Kwa
mujibu wa Makongoro, hali hiyo imechochea badhi ya viongozi wa CCM
katika ngazi mbalimbali wakiwamo wenyeviti wa mikoa na wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya chama hicho kuishi kama mifugo.
Alisema
hali hiyo imesababisha baadhi ya viongozi hao kuishi maisha ya
kusukumwa kwa upepo wa makundi yanayomilikiwa na watoa fedha.
“Vibaka waturudishie CCM yetu, watambue wao ni wachache na sisi wazalendo ni wengi, hawatushindi na fedha zao na kitaeleweka tu.
“Leo
hii viongozi wetu wa CCM wamekuwa ni watu wa kuendeshwa na vibaka hawa
wanahongwa fedha ovyo…wao wana mifugo yao ndani ya NEC basi mimi
sijafuga hata kuku, nasema kitaweleweka,” alisema Makongoro.
Alisema
yeye hawezi kufanya hivyo kwa sababu rasimu ya ilani ya chama hicho
bado haijapitishwa na chama, hofu yake ni kwamba anaweza kutoa ahadi na
zikawa kinyuume na ilani ya chama chake.
“Nimewasikia
wanajinadi,nawashangaa sana, najiuliza kwani wao ni akina nani watoe
ahadi kabla ya ilani ya chama? Ikitokea ahadi yako ikaenda kinyume na
ilani si ndiyo mwanzo wa kuwa na rais muongo…sitaki kuwa rais muongo
nitaheshimu chama changu kwa kila mchakato na maelekezo,” alisema Makongoro.
Aliwaasa Watanzania wawaogope watu wanaoonekana kuwa na haraka ya kukimbilia kutawala nchi.
“Ukiona
watu kazi inatangazwa ifanywe kwa utaratibu wake na mtu aliyeiomba kazi
hiyo anakiuka taratibu, muogopeni sana huyo hafai kukukuongoza maana
hata akikuongoza ataendelea kukiuka taratibu ili ajinufaishe,” alisema Makongoro.
Wanawake wananipenda
Makongoro alisema anakerwa na siasa chafu dhidi yake zinazoenezwa na baadhi ya wanasiasa wenzake ndani ya CCM.
Alizitaja siasa hizo kuwa ni tuhuma za kulaaniwa na baba yake, ulevi na mtu anayependa wanawake.
Akijibu tuhuma hizo, Makongoro alihoji umati uliomiminika kumsikiliza kwamba, “jamani
naonekana nimelaaniwa? Naelekea kuokota makopo? Jamani mnanionaje,
naonekana mlevi? na umati ulikataa kwa kusema, “hapana”.
“Eti
wanasema Makongoro anapenda wanawake sasa wanataka nipende wanaume?
Wanawake wananipenda na mimi nawapenda, hizi siasa chafu wanazonituhumu
hazinisumbuilangu ni moja tu vibaka rudisheni nchi yetu,” alisema.
Nimrod Mkono
Naye
Mbunge wa Musoma Vijijini , Nimrode Mkono alisema atakuwa bega kwa bega
na Makongoro kuanzia sasa katika safari yake ya kuwania urais mpaka
hatua ya mwisho.
“Wapo
wengi walionifuata niwe nao katika harakati zao za kuwania urais, sasa
nawaambia ‘bye bye’ nipo na Makongoro na wasijihangaishe kunitafuta,” alisema Mkono.
Shyrose
Mbunge
wa Bunge la Afrika Mashari, Shyrose Banji na mwanamuziki wa kizazi
kipya, Judith Wambura ‘Lady J Dee’ nao walihudhuria kikao hicho.
Makongoro afananishwa na Daudi
Awali
kabla ya Makongoro kutangaza nia ya kugombea urais,baadhi ya viongozi
wa dini walimuombea ambako Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Jackob
Ngagani alimfananisha na Daudi.
Alisema anaamini Mungu atamuongoza Makongoro kushinda ushindani wa kupata mgombea urais kupitia CCM.
Kabla
ya dua ya viongozi wa dini, wazee wa kabila la Wazanaki, walimvisha
vazi la asili la kabila hilo na kumkabidhi fimbo kwa ajili ya kuwaongoza
Watanzania.
Naye Chifu wa Kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi alisema Makongoro ni simba na kusisitiza kuwa kabila lao huwa halibahatishi.
Post a Comment