INAUMA
sana! Aisha Ally mwenye umri wa miaka 8 (pichani), mkazi wa Mtaa wa
NSSF, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam ambaye pia alikuwa mwanafunzi wa
darasa la tatu wa Shule ya Msingi ya St. Joseph, Dar, amefariki dunia
baada ya kung’atwa na mbwa anayedaiwa kuwa na kichaa, Uwazi lina mkasa
wote.
Tukio hilo lilijiri hivi karibuni
nyumbani kwao Mbezi wakati mtoto huyo alipotumwa na mama yake mkubwa
kwenda dukani kununua vocha ya simu.Akisimulia tukio zima kwa waandishi
wetu, baba mzazi wa marehemu, Ally Ayub alisema:
“Siku ya tukio mwanangu alitumwa na mama
yake mkubwa kwenda dukani kumnunulia vocha, sasa wakati anarudi
nyumbani njiani alikutana na mbwa huyo akamshambulia kwenye mguu wa
kushoto, mkono wa kushoto na mdomoni.
“Mwanangu alijitahidi kupambana naye ili kujiokoa lakini mbwa naye alikuwa na nguvu, akamng’ata sehemu hizo.”
“Baadhi ya watu waliokuwepo dukani
waliona, wengine walianza kulia baada ya kumtambua mwanangu, wengine
walikimbilia eneo la tukio kwa lengo la kumwokoa, mmoja wao alimpiga
teke yule mbwa akatokomea kusikojulikana.
“Ndipo yule mtu aliyempiga teke mbwa na
watu wengine walimleta mwanangu nyumbani akiwa anavuja damu sehemu
alizong’atwa. Niliumia sana! Na bado nikikumbuka naendelea kuumia.”
Mzazi huyo alisema kwamba, kabla ya
kumkimbiza hospitali Aisha, alimpaka dawa aina ya spiriti kwa lengo la
kumkausha damu.Aliendelea kusema: “Baada ya hapo tulimkimbiza Hospitali
ya Muhimbili, tulipokelewa vizuri lakini cha ajabu hata dawa aina ya
yuso tuliambiwa tukanunue nje jambo lililotusikitisha sana.
“Shida kubwa ilikuwa ni mtoto wangu
atibiwe hivyo jirani yangu aliyenisaidia gari pamoja na kunisindikiza,
alikwenda kununua hiyo yuso, akapakwa na kuchomwa sindano moja,
akafungwa majeraha kisha tukaambiwa turudi nyumbani na kupangiwa tarehe
nyingine ya kurudi.”
Akiendelea kusimulia mkasa huo kwa masikitiko makubwa huku machozi yakimtiririka, mzazi huyo alisema:
“Kumbe kiutaratibu mwanangu alipaswa
achomwe sindano nyingine baada ya saa 72 kitu ambacho hakikufanyika wala
kushauriwa na wataalam wa hospitali hiyo.
“Baada ya kurudi nyumbani tulishauriana
na mke wangu kwamba mwanangu akakae kwa shangazi yake Kibamba kutokana
na shughuli zetu kutofautiana, hivyo muda wa kukaa na mtoto mgonjwa
ulikuwa finyu.”“Siku chache baadaye nikiwa safarini, nilipigiwa simu na
mke wangu, akaniambia amepigiwa simu na wifi yake (Salima) na kumwambia
kwamba, Aisha anaumwa.
“Alisema alimpeleka hospitali akapimwa na kukutwa ana malaria 2 hivyo alianzishiwa dozi ya dawa ya mseto.
“Siku mbili mbele nikiwa nimerejea
kutoka safari, shangazi wa mtoto alinipigia simu na kunifahamsha kwamba
Aisha alikuwa anashtukashtuka.
“Kesho yake nilikwenda kumchukua,
nikampeleka Muhimbili kwa maana ya kutibiwa. Ilikuwa majira ya saa sita
mchana, akalazwa Wadi B, Chumba J, Jengo la Watoto kisha akapewa vidonge
vya kutuliza maumivu.”
“Kesho yake saa sita usiku, siku ya
Ijumaa hali ya mtoto wangu ilizidi kuwa mbaya, akawekewa dripu lakini
hali iliendelea kuwa mbaya, akahamishiwa Chumba I ambako tulikaa naye
kwa takriban saa moja tu, akafariki dunia.” Machozi yakamtoka.Marehemu
Aisha alizikwa saa 9 alasiri Aprili 27, mwaka huu kwenye Makaburi ya
Ngazija yaliyopo Kisutu jijini Dar. GPL
Post a Comment