Serikali imeandaa zaidi ya mashahidi 15 kwa ajili ya kutoa ushahidi kwenye kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja.
Minja
alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Dodoma jana na kusomewa
maelezo ya awali ya kesi inayomkabili. Alikana mashtaka yote mawili ya
uchochezi mbele ya Hakimu Rhoda Ngimilanga.
Mwendesha
Mashtaka wa Serikali, Paul Kadushi alidai kuwa Septemba 6, 2014,
mshtakiwa akiwa katika Chuo cha Mipango kilichopo Kata ya Miuji,
Manispaa ya Dodoma, alitoa kauli zilizochochea kutendeka kwa kitendo cha
jinai kinyume na sheria.
Katika
kosa la pili siku hiyohiyo, mshtakiwa alitenda kosa kwa kuzuia
ukusanyaji wa kodi kwa kuwachochea wafanyabiashara nchini kutotumia
mashine za kielektroniki za kukusanya kodi (EFDs).
Hata hivyo, Minja alikubali baadhi ya maelezo yaliyotolewa baada ya kusomewa na wakili huyo wa Serikali.
Alikubali
mahakamani kuwa anatambua kuwapo na sheria ya matumizi ya mashine za
kielektroniki kwa ajili ya kukusanyia kodi, sheria ya kukusanya kodi na
utambulisho wake uliotolewa mahakamani.
“Ni
kweli kuwa Septemba 6 mwaka jana, tulifanya mkutano katika Chuo cha
Mipango kwa lengo la kuwapa wafanyabiashara mrejesho wa maendeleo ya
mazungumzo yetu na TRA kuhusu matumizi ya EFD ili kuiongezea Serikali
mapato bila kuua uchumi wa nchi na mfanyabiashara mwenyewe,” Minja.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 8 na itasikilizwa kwa siku tatu mfululizo hadi Juni 10.
Post a Comment