Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema amesema hakuna ubaya Rais Jakaya Kikwete akiachwa kuongoza nchi kwa muda ili akamilishe mchakato wa Katiba Inayopendekezwa pamoja na Daftari la Kudumu la Wapigakura.
Hivi karibuni viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), walidai kuwa Serikali na Tume ya Uchaguzi (NEC) inachelewesha
uboreshaji wa Daftari la Wapigakura kwa lengo la kutaka kumwongezea Rais
Kikwete muda wa kukaa Ikulu.
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema ni miezi mitatu imebaki kabla ya
kampeni za uchaguzi, lakini mpaka sasa ratiba, majimbo yaliyogawanywa,
watumishi wala vituo vya uchaguzi bado haviwekwa bayana na wala
haifahamiki kazi ya uandikishaji katika Daftari la Wapigakura
halijakamilika katika mikoa miwili.
“Hiyo
ni hatari sana kwa Taifa. Tunaionya NEC isijaribu kufanya mbinu
zitakazosababisha kuahirishwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu,” alisema Mbowe.
Akizungumza
na mtandao huu jana, Mrema alisema yeye ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza
kutoa wazo la kutaka Rais Kikwete aongezewe muda zaidi wa kukaa Ikulu
kwa kuwa kuna mambo mengi ambayo ni ya muhimu kwa Taifa yanayotakiwa
kukamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu.
Mrema alisema alitoa maoni hayo mwaka jana wakati viongozi wa Kituo
cha Demokrasia Tanzania (TCD) walipokutana na Rais Kikwete mjini
Dodoma, lakini alishangaa kuona viongozi wengine wakipinga wazo hilo.
“Nilitoa
ushauri Rais Kikwete akiwepo. Nilisema tusogeze Uchaguzi Mkuu mbele kwa
miaka miwili ili atuachie nchi ikiwa salama, lakini wapinzani
wamejiandaa kuingia Ikulu waliniona mimi kama bundi,” alisema Mrema.
Aliongeza
kuwa hata Rais Kikwete hakuonekana kufurahishwa na hali hiyo
iliyojitokeza baada ya kauli yake na kwamba, hivi sasa amebaini kuwa
kiongozi huyo wa nchi hataki kuongezewa hata siku moja ya kuendelea
kukaa Ikulu.
“Sema kwa sababu wenzangu wamejiandaa kuingia Ikulu mwaka huu, wameshawaandaa hata wake zao kuwa ‘ma-first lady’, lakini ukweli ni kwamba hata Katiba Inayopendekezwa ikipitishwa lazima kuwe na muda wa mpito.
“Simfanyii
mtu kampeni, ninachosema ni kwamba, mambo hayajakamilika na tunataka
yakamilike na michakato yote aliyeianzisha ni Rais Kikwete, ni vyema
akaimaliza,” alisema Mrema.
Akihutubia
kwenye sherehe ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani jijini
Mwanza juzi, Rais Kikwete alisema hana mpango wa kuongeza muda kama
baadhi ya wanasiasa wanavyodai.
“Nawashangaa
wanaodai kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza muda wa urais, sina
mpango wa kufanya hivyo, tarehe imepangwa na uchaguzi utafanyika kwa
mujibu wa Katiba,” alisema Rais Kikwete.
Post a Comment