WAFANYABIASHARA wadogo na waendesha bodaboda wanaofanya biashara zao kwenye njia kubwa za kusafirishia umeme wapo hatarini kupungukiwa nguvu za kiume.
Kutokana
na kuwepo wengi kwenye njia hizo kubwa za kusafirishia umeme,
wametahadharishwa kutoendelea kufanya biashara kwenye maeneo hayo.
Hayo
yalibainishwa jana na Ofisa Mahusiano Msaidizi huduma kwa wateja wa
Tanesco Mwanza, Haji Bwegege wakati akizungumza na waandishi wa habari
baada ya uzinduzi wa maonyesho ya siku ya wafanyakazi uliofanywa na
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo kwenye viwanja vya Furahisha,
jijini hapa.
“Tumekuwa tukiielimisha jamii mara kwa mara kutofanya biashara kwenye njia ya umeme mkubwa unaopita kutokana
na madhara wanayoweza kuyapata na hii ya kupungukiwa nguvu za kiume ni
moja ya madhara ambayo yanaweza kuwapata hivyo wachukue tahadhari
mapema,” alisema.
Aliyataja
madhara mengine kuwa pamoja na mwili kupoteza nguvu kutokana na mionzi
hivyo wananchi kutakiwa kuishi umbali wa mita 30 kila upande pamoja na
mjamzito kuharibu mimba.
Akizungumzia
suala la ‘Vishoka’, Bwegege aliwataka wananchi wasikubali kuuziwa fomu
majumbani kwani fomu za kuomba kuunganishiwa umeme hutolewa ofisini tu
ama pale maofisa wao wanapotembelea vijijini wakiwa na vitambulisho na
kutoa risiti.
“Mnatambua kuwa miradi ya umeme vijijini inaendelea ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Electricity
five (F5) hivyo vishoka kutumia nafasi hiyo kuwarubuni wananchi ambapo
wamekuwa wakifika vijijini na kuwauzia fomu kati ya Sh 60,000 na 100,000
wakati bei halisi ya fomu ni Sh 5,900 tu,”alisema.
Alisema
vishoka hao wamekuwa wakijitokeza katika maeneo ya vijijini ambapo
miradi hiyo imekuwa ikiendelea na kwamba kama Tanesco wamekuwa
wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kufanya mikutano ya hadhara na kuwataka wananchi wajiandikishe kwenye ofisi za serikali za vijiji.
Bwegege alisema chini ya miradi ya wakala wa umeme vijijini, wananchi wanaozungukwa na mradi hutozwa Sh 27,000 kama gharama ya kuungiwa umeme.
Alisema
wameshiriki katika maonesho hayo ili kutoa elimu kwa jamii juu ya
shughuli zao na kwamba huduma zote zinazotolewa ofisini zinatolewa
uwanjani hapo.
Post a Comment